Jumamosi, 5 Aprili 2014

Sigara huharibu DNA mwilini na kuongeza hatari ya kupata kensa!




Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu DNA za mwili wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na kuongeza uwezekano wa mtu kupata kensa. Katika uchunguzi huo watalamu walichukua kemikali hizo katika miili ya wavuta sigara na kuzifanyia uchunguzi, ambapo waligundua kuwa, kemikali za PHA hubadilika haraka mwilini na kuwa sumu ambayo huharibu DNA baada ya kupita dakika 15 hadi 30 tangu kuingia tumbaku katika mwili wa binadamu. Sumu hiyo hubadilisha seli mwilini au kufanya mutation, kitendo ambacho huweza kusababisha kensa. Wataalamu hao wanasema, kitendo hicho hufanyika kwa haraka sana kama vile inavyoingizwa mada ya sumu kwenye damu kwa sindano. Habari hii ni tahadhari kwa watu wanaotaka kuanza kuvuta sigara, kwani takwimu zinatuonyesha kwamba, watu 3,000 hufariki dunia kila siku umwenguni kutokana na kensa ya mapafu, maradhi ambayo husababishwa kwa asilimia 90 na uvutaji sigara. Madhara ya kuvuta sigara kwa muda mrefu yanajulikana na wengi, ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kensa mbalimbali, lakini wataalamu wanatuasa ya kuwa, madhara ya sigara huanza pale tu mtu anapoanza kupiga pafu ya kwanza na kuingiza moshi wa sigara mwilini. Hivyo bado hujachelewa na unaweza kuacha sigara hii leo!

Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu.



Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua
Watoto wadogo hasa wale ambao bado wananyonya na ndio kwanza wamenzishwa vyakula vinginevyo zaidi ya maziwa, mara nyingi hupatwa na choo kigumu au kukosa choo kabisa hali tunayoiita kimombo, constipation. Hali hiyo huanza pale mtoto anapoachishwa maziwa ya mama na kuanza kunyweshwa maziwa ya kopo au mengineyo au pia anapoanzishwa kula vyakula vingine zaidi ya maziwa. Mara nyingi watoto wanaonyonya maziwa ya mama huwa hawasumbuliwa na tatizo hilo, bali tatizo hilo huanza kujitokeza pale wanapoanza kulishwa vyakula vingine zaidi ya maziwa ya mama. Pia mama ambaye tayari mwenyewe anasumbuliwa na tatizo la kukosa choo, huenda mwanae pia akasumbuliwa na tatizo hilo.
Mtoto mwenye tatizo la kukosa choo huwa anapata choo wa shida huku akisumbuliwa na tumbo na kupata choo kigumu. Wakati mwingine hulia wakati akipata choo huku akijiminya na kukunja uso. Muone daktari iwapo mtoto ana umri wa chini ya mwezi mmoja na hajapata choo kwa siku 4.

Neno 'Afya' linamaanisha nini?



Kwa mujibu wa  ufafanuzi uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO katika mkutano wake wa tarehe 19-22 Juni 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani, 'afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili na kijamii na sio tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu.' Ufafanuzi huo ulianza kutumika Aprili mwaka 1948 na hadi hii leo maana hiyo ya afya haijabadika. Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba, tunaposema mtu ana afya sio tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi, upungufu au udhaifu bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na matatizo ya kimwili, kiakili na hata kijamii. Kwa mujibu wa tafisri hiyo pana ya neno 'afya' tunaona kuwa watu wengi wanaamini kuwa afya imeganyika katika makundi mawili muhimu ambayo ni afya ya kimwili na afya ya kiakili. Afya ya mwili kwa binaadamu ina maana, kuwa na mwili wenye afya usiokuwa na maradhi, afya ambayo kwa kawaida hutokana na kuupa mwili mazoezi ya mara kwa mara, lishe bora na mapumziko ya kutosha. Katika nchi au maeneo ambayo watu wanapata lishe bora, huduma nzuri za afya na kuishi katika hali ya kimaisha inayoambatana na viwango vinavyotakiwa, kwa kawaida vimo na uzito wao huongezeka. Ukweli ni kuwa, ukiwauliza watu wengi afya ni nini, watasema kwamba inahusiana na  mwili kuwa salama bila ya kuathirika na ugonjwa. Lakini tukienda ndani zaidi, kitiba afya ya mwili inaamanisha ustawi wa mwili hali ambayo mtu anaipata kwa kutekeleza vipengee vyote vinavyohusiana na afya katika maisha yake. Uzima wa mwili unaakisi kufanya kazi vizuri moyo na mfumo wa kupumua, uwezo wa misuli, viungo pamoja na mwili kuweza kukubali mabadiliko tofauti na muundo wa mwili kwa ujumla. Masuala mengine ni pamoja na lishe bora, uzito wa mwili, kutokuwepo uraibu wa madawa ya kulevya, pombe, mahusiano salama ya kimwili, usafi kwa ujumla na pia kulala na kuamka kwa wakati unaotakiwa.

 Afya ya akili au uzima wa kiakili ni utambuzi wa mtu na uzima wake kisaikolojia. Mtu ambaye ana afya nzuri ya kiakili hana matatizo ya kiakili au kichaa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, 'afya ya akili ni pale mtu anapoweza kufahamu uwezo wake na kustahamili mfadhaiko (stress) unaotakana na dhiki au matatizo ya kawaida ya kimaisha. Aweze kufanya kazi yenye kuleta mafanikio na kuchangia masuala tofauti katika jamii yake.'

Ni rahisi watu kuelezea maana ya ugonjwa wa akili kuliko afya ya akili. Watu wengi wanakubali kwamba afya ya akili ni kutokuwepo ugonjwa wa akili lakini maana hiyo haitoshi. Hii ni kwa sababu kama tutachagua watu 100 ambao hawana kichaa au ugonjwa wa akili unaoweza kutambuliwa na daktari wa akili, lakini miongoni mwao tunaweza kuona kwamba afya ya baadhi yao kiakili imeimarika kuliko wengine.Tunaweza kusema kuwa, afya ya akili inajumuisha masuala kadhaa kama vile uwezo wa kuishi kwa furaha, uwezo wa kuvumilia shida na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kupatwa na matitizo, uwezo wa kuwa na uwiano katika maisha,  uwezo wa kubadilika kwa urahisi na kuzoea mazingira mapya, kujihisi salama na kujitambua.

KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NASI KWA +255762285404 AU +255713354389



Jumamosi, 11 Januari 2014

MATUMIZI YA CHUMVI NYINGI NI HATARI.

Miili yetu inahitaji chumvi kiasi kidogo sana. Kwa wastani tunahiaji kama gramu 1.25 (kama robo kijiko cha chai) kwa siku. Kwa bahati mbaya tunatumia chumvi kupita kiasi. Wataalamu wa Afya wanahusisha matumizi ya chumvi nyingi na uwezekano wa kupata msukumo mkubwa wa damu (High Blood Pressure), ambayo pia inaongeza uwezekano wa kupata magonjwa mengine sugu kama yale ya figo, moyo, ikiwepo “stroke” na pia ya mifupa kama “osteoporosis”.

Hivi karibuni tafiti zimeonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya vyakula vyenye chumvi nyingi na saratani ya tumbo.
Sasa kazi kwetu!! Tujitahidi kupunguza uwezekazo wa kupata magonjwa sugu. Pungunguza matumizi ya chumvi na vyakula vyenye chumvi nyingi. Yafuatayo yatasaidia kufikia lengo hilo:
  • Punguza chumvi inayowekwa kwenye chakula wakati wa kupika.
  • Usiweke chumvi mezani (wengine huongeza hata bila kuonja chakula)
  • Epuka vyakula vilivyosindikwa kwa kutumia au kuongezwa chumvi
  • wapo unanunua vyakula vilivyosindikwa, kama vya makopo au paketi, soma lebo kwa makini. Chagua vilivyoandikwa “hakuna chumvi iliyoongezwa”(“no salt added”)
  • Tumia zaidi vyakula freshi unavyopika mwenyewe kwani unaweza kuthibiti kiasi cha chumvi unachotumia.
Kama tayari umezoea kutumia chumvi nyingi itakuchukua muda kidogo kujizoesha chakula chenye chumvi ndogo au kisicho na chumvi. Jizoeshe kidogo kidogo na utazoea, tena utafurahia vyakula vyenye chumvi kidogo au visivyo na chumvi.

Kumbuka ni maisha yako na ufunguo wa kuingia katika mtindo bora wa maisha upo mkononi mwako. Jipende!

UZITO ULIOPITA KIASI NI HATARI KWA AFYA YAKO.



Uzito uliozidi kiasi unakuweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mengi sugu kwa mfano, kisukari, msukumo mkubwa wa damu, magonjwa ya moyo, figo, saratani na mengineyo. Magonjwa haya yanaleta kifo mapema na matatizo mengine mengi…. Jizoeshe taratibu za kula ambazo zitakusaidia kupunguza uzito au kuzuia ongezeko kubwa la uzito..Badili mtindo wa kula, yafuatayo yanaweza kukusaidi:
  • Jaribu kutumia sahani ndogo, na usichote chakula mara ya pili (usiongeze), watafiti wameona kwamba mtu anayetumia sahani kubwa mara nyingi anakula chakula kingi kuliko akitumia sahani ndogo.
  • Nusu au zaidi ya mlo uliochotea kwenye sahani iwe ni vyakula vinavyotokana na mimea hasa mboga mboga.  Kama unakula “sandwich” ya mkate, kula nusu na ongezea kwa mbogamboga na matunda.
  • Asubuhi ule mlo wa kushiba zaidi na jioni ule chakula kidogo/chepesi (usishibe sana usiku).
  • Usile kwa haraka, mara nyingi unapokula kwa haraka unakula chakula kingi na pia chenye nishati nyingi.  Ongeza vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi kama mbogamboga, nafaka zisizokobolewa (whole-grains), mara nyingi vyakula hivi huwezi kula haraka wala huwezi kula kupita kiasi.
  • Jipe muda wa kutosha kutafuna vizuri, na mara nyingi vyakula bora kama ugali wa dona, mkate wa brauni, mahindi ya kuchoma au kuchemsha, maharage, kunde huhitaji kutafunwa vizuri hivyo huwezi kula kupita kiasi.
  • Epuka asusa zenye mafuta mengi, sukari nyingi au chumvi nyingi.  Jizoeshe matunda, hindi la kuchoma au vyakula vingine vya aina hiyo.
  • Jipe muda kujitayarishia mlo ulio bora wenye mboga mboga nyingi.  Kumbuka ni uhai wako. Labda umetumia dakika 10 zaidi kutayarisha mlo lakini imekuepusha kutumia siku nzima au zaidi kwa daktari na kulipa gharama kubwa.
  • Epuka kutumia vyakula vilivyotengenezwa kwa haraka (fast food) kwenye migahawa, mara nyingi vina mafuta mengi, chumvi nyingi au sukari nyingi.  Na pengine unaona umekula asusa (snack) tu, kwa hiyo unakula tena mlo mzima.  Kwa mfano watu wengine husema “I grabbed something” kwa maana hajala vizuri kumbe ni kwa kuwa alikula bila mpango.
  • Epuka kula ukiwa unaangalia TV, unatumia computer au unafanya shughuli nyingine kwani una hatari ya kula kupita kiasi.
  • Tuwazoeshe watoto ulaji bora unaoshirikisha mbogamboga na matunda, na aina za kunde, nyama kwa kiasi. Epuka kummzoesha chumvi nyingi, mafuta mengi au sukari nyingi. Akishazoea itakuwa shida kuacha. Mpende mwanao, mfundishe vitu vitakavymrefushia maisha.
  • Epuka pombe na sigara
  • Fanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 au zaidi kila siku, hata kutembea tu.
  • Kumbuka mwili wako unatokana na unachokula na mazoezi unayofanya

Alhamisi, 12 Desemba 2013

HAMIRA NA MADHARA YAKE KWA KINYWA NA KOO

Leo hii tunaangalia maradhi ya fangasi aina ya hamira (yeast) yanayoshambulia kinywa na koo ambayo kwa kitaalam ,oral candidiasis. 

Utando wa kinywa (Oral Candidiasis)

Utando huu wa kinywa ni maradhi yanayosababishwa na fangasi aina ya hamira ambao hushambulia eneo la ndani la kinywa na koo la kumezea chakula.

Fangasi hawa hushambulia kinywa na koo kwa hali ya kawaida na huwa na makazi yao kwenye maeneo haya pamoja na sehemu mbalimbali katika mfumo wa mmeng`enyo wa chakula na pia hupatikana kwenye ngozi.

Kinga ya mwili wa binadamu pamoja na vimelea vinavyokaa mwilini aina ya bakteria huzuia fangasi hawa wasiongezeke kiasi cha kugeuka na kuanza kushambulia maeneo hayo ya koo na kinywa.

Hata hivyo, inapotokea uwiano huu wa kinga ya mwili na bakteria kushindwa kuzuia ongezeko la fangasi, basi fangasi hao huongezeka na kuwa wengi na hapo ndipo husababisha utando ambao huonekana kwenye kinywa na hata koo la chakula la mgonjwa.

Sababu za maradhi

Idadi kubwa  ya fangasi aina ya kandida (candida) katika maeneo ya kinywa na koo husababisha utando huu.

Jinsi na nani hushambuliwa

Maradhi haya ni kawaida kuonekana kwa watoto wachanga. Maradhi haya yanatokea zaidi kwa watoto wachanga kutokana na hali ya kutokuwa na uwiano sahihi kati ya kinga ya mwili wa mtoto, aina ya bakteria pamoja na fangasi hawa wanoitwa kandida.

Maradhi haya pia huweza kutokea kwa watu wazima na mara zote hutokea baada ya kutokea mabadiliko yaliyosababisha kuvurugika kwa uwiano kati ya kinga ya mwili, bakteria walioko kwenye eneo la kinywa na koo pamoja na vimelea vinavyosababisha utando huu, yaani kandida.

Viashiria hatarishi

Viashiria hatarishi vinavyomweka mtu kwenye hatari ya kupata maradhi haya vinafanana kabisa na sababu zinazomfanya mtu kupata maradhi haya.

Maradhi haya kwa kawaida kama nilivyoeleza hushambulia watoto wachanga, inapotokea yakatokea kwa mtu mzima basi mara nyingi lazima kuwe kuna viashiria hatarishi kama vifuatavyo:

-Watu wenye upungufu wa kinga kwa sababu yoyote ile wako kwenye hatari ya kupata maradhi haya. Mfano, watu wenye maradhi ya muda mrefu kama saratani, kisukari na yale yanayosababisha kinga kushuka kama Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi).

-Wanawake wajawazito (Ujauzito huweza kusababisha kinga kushuka)

-Watu wanaokunywa dawa kwa muda mrefu, hususan dawa za antibaiotiki, dawa za kutibu saratani na dawa za maradhi mengine ya muda mrefu.

-Sonona na msongo wa mawazo wa muda mrefu (hushusha kinga pia)

Je, maradhi haya huambukiza?

Maradhi haya si ya kuambukiza ingawa mtoto mchanga mwenye maradhi haya huweza kusambaza maradhi kwenda kwenye titi la mama kwa njia ya kugusa moja kwa moja wakati wa kunyonya.

Jumapili, 8 Desemba 2013

KULA NYANYA UJIEPUSHE NA KIHARUSI



SOTE tunajua ugonjwa wa kiharusi (stroke) ni miongoni mwa magonjwa hatari kwani ukikupata unaweza kudhoofisha baadhi ya viungo vyako vya mwili kama siyo vyote na kukufanya ushindwe kufanya kazi zako za kawaida na kuwa mtu wa ndani tu kwa maisha yako yote.

Lakini unaweza kujiepusha na ugonjwa huo hatari kwa kuzingatia ulaji wa vyakula sahihi pamoja na kufanya mazoezi. Utafiti wa hivi karibuni umebaini kwamba nyanya (tomatoes) hutoa kinga mwilini dhidi ya ugonjwa wa kiharusi au kupooza kama unavyojulikana na wengine.
Hivi karibuni, watafiti wa nchini Finland walifanya utafiti wa kina na kutoa taarifa kuhusu kirutubisho aina ya ‘lycopene’ kinachopatikana kwa wingi kwenye nyanya, matikitimaji na pilipili. Wamesema katika taarifa yao kuwa watu zaidi ya 1,000 waliowafanyia utafiti wenye kiwango kingi cha ‘lycopene’ kwenye mfumo wa damu zao, hawakuonesha dalili kabisa za kupatwa na kiharusi.
Aidha, Chama cha Taifa cha wenye Kiharusi cha nchini Marekani (The National Stroke Association) kimesema kuwa wanawake wengi hufariki dunia nchini humo kutokana na kiharusi kwa idadi sawa na wale wanaofariki kutokana na ugonjwa wa saratani ya matiti. Hii ina maana kwamba ugonjwa wa kiharusi nao ni tishio kama ilivyo kwa ugonjwa wa saratani ya matiti.
Utafiti mwingine katika eneo hilo umeonesha pia kuwa wanaume wana hatari kubwa zaidi ya kufariki dunia au kupatwa na matatizo mengi kutokana na ugonjwa wa kiharusi kuliko wanawake. Hivyo kati ya wanaume na wanawake, wanaume zaidi ndiyo hupatwa na kiharusi au matatizo yatokanayo na ugonjwa huo kuliko wanawake.

Utafiti huu mpya umeendelea kuthibitisha ukweli wa siku zote kuwa matunda na mbogamboga hutoa kinga katika mwili wa binadamu dhidi ya magonjwa mengi hatari, hivyo wito umetolewa tena wa watu kupenda kula matunda na mbogamboga hasa nyanya, matikitimaji pamoja na pilipili ambavyo vimeonekana kuwa na kinga kubwa zaidi mwilini.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa baada ya matokeo ya utafiti huu, watu wamekumbushwa umuhimu wa kuendelea kula na aina nyingine ya matunda, kwani kila tunda au mboga ya majani ina faida na umuhimu wake katika mwili wa binadamu.



Mwisho imeelezwa kuwa ulaji wa nyanya kwa siku zaidi ya 50 za aina zote una faida, ile inayoliwa ikiwa imeiva bila kupikwa. Ni vizuri kuchangamkia ulaji wa vitu kama hivi ili kuipa miili yetu uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi hatari, yakiwemo yale ya saratani, kansa ya tezi dume ambayo kwa kiasi kikubwa huweza kuzuiwa kwa kula mboga za majani na matunda ya aina mbalimbali, pamoja na nyanya 50 kwa siku zilizoiva vizuri au kupata FOOD SUPPLIMENT ZINAZOTENGENEZWA KWA KIWANGO HICHO CHA NYANYA NA MCHANGANYIKO WA MATUNDA MBALIMBALI.