Kwa baadhi ya wanaume wanaugua ugonjwa
huo kuliko wanawake
Ukitembea katika jamii hasa mijini utawasikia watu wengi hasa
wanaume wanapokunywa bia na kula supu wakizungumzia ugonjwa huu wanaoutaja kama
gauti. Unaweza kujiuliza, huu ni ugonjwa gani?
Huu ni ugonjwa unaoathiri viungo vya mwili
unaosababishwa na kuwepo kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida cha tindikali aina ya
uriki (uric acid) katika damu.
Ongezeko hilo la uriki husababisha madhara katika viungo vya
mifupa, viungo ni sehemu ya mwili inapokutana, inapoungana mifupa miwili. Kwa
kawaida, gauti inaweza kutokea ghafla au ikawa sugu.
Kwa ile inayotokea ghafla huwa na maumivu makali na mara nyingi
huathiri kiungo kimoja tu wakati gauti sugu inaweza kuathiri kiungo zaidi ya
kimoja na huambatana na hali ya kujirudia ya maumivu na uvimbe kwenye viungo.
Visababishi vyake
Gauti husababishwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida
cha tindikali ya uriki katika damu. Hali hii hutokea iwapo mwili wa
mgonjwa unatengeneza uriki nyingi kuliko kawaida au unashindwa kutoa
tindikal ya uriki mwilini kama inavyotakiwa.
Ongezeko hili husababisha mrundikano wa tindikali ya uriki
katika majimaji yanayozunguka viungo yanayoitwa synovial na hatimaye kutengeneza
vijiwe vidogovidogo vya tindikali ya uriki ambavyo husababisha viungo kuvimba
na hatimaye kuathirika.
Vihatarishi
Ingawa chanzo halisi hakieleweki vyema, ugonjwa hutokea kuwapata
baadhi ya watu walio wa familia moja. Wanaume huathiriwa zaidi kuliko wanawake
ingawa wanawake waliokoma kupata hedhi huathiriwa zaidi.
Aidha, unywaji pombe unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa
ugonjwa huu pamoja na matumizi ya baadhi ya dawa kama vile za kutoa maji
mwilini ambazo kwa ujumla husababisha ongezeko la kiwango cha uriki katika
damu.
Vihatarishi vingine ni pamoja na kuwa na ugonjwa wa kisukari,
magonjwa ya figo, unene uliokithiri, upungufu wa damu unasababishwa na seli
mundu (sickle cell) au aina nyingine za upungufu wa damu, pamoja na
saratani ya damu (leukemia).Pia, gauti inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa
ambazo utendaji wake kazi huingiliana na utoaji wa tindikali ya uriki mwilini.
Dalili za ugonjwa huo
- Dalili kwa kawaida huhusisha kiungo kimoja au vichache. Viungo
vinavyoathiriwa zaidi ni pamoja na kidole kikubwa cha mguuni, magoti, au kiwiko
cha mguu.
-Wagonjwa huwa na maumivu yanayoanza kwa ghafla, hususan nyakati
za usiku. Mara nyingi mgonjwa hudai anasikia maumivu makali kama kitu
kinachokata, kupwita au mifupa inayosagana.
-Viunganio katika mwili hubadilika na kuwa na joto, kuvimba na
kuwa na nyekundu (hujionyesha zaidi kwa watu wenye ngozi nyeupe). Kwa kawaida
mgonjwa hulalamika maumivu makali ikiwa ataguswa kwenye kiungo chenye matatizo.
-Shambulio linaweza kudumu kwa siku kadhaa kabla mgonjwa
hajapata nafuu, pia laweza kujirudia mara kwa mara.
-Pia mgonjwa anaweza kujihisi homa. Baadhi ya wagonjwa hupata
gauti sugu ambayo huwaletea madhara sugu katika viungo (chronic arthritis) hali
ambayo husababisha mgonjwa kujihisi maumivu na muda mwingi kushindwa vizuri
kutumia viungo vyake.
Wagonjwa wa muda mrefu huwa pia na vinundu chini ya ngozi
inayozunguka viungo vilivyoathirika. Vinundu hivi ni ishara ya muhimu kwa
madaktari.
Ushauri:
-Tuache pombe
-Tupunguze ulaji wa vyakula vyenye viasili vya purine (aina ya
protini) kama vile nyama ya mbuzi, samaki jamii ya sardines na herring, maini
au figo, mkate mtamu, maharage yaliyokaushwa, njegere, baadhi ya uyoga,
spinachi. Dhibiti pia ulaji wa nyama kwa kila mlo.
Jiepushe na matumizi ya vyakula vya mafuta kama vile ice creams,
mayonise au vyakula vya kuokwa. Kula kiasi kikubwa cha wanga. Iwapo utaamua
kupunguza uzito, hakikisha unapunguza kidogo kidogo kwa sababu upunguzaji wa
kasi unaweza kusababisha vijiwe vya uric kujitengeneza katika figo.